PHIRI: KWA OKWI,SSERUNKUMA MTALALA NA VIATU.

KOCHA wa Simba, Patrick Phiri, amesema atakuwa na kikosi cha kwanza cha uhakika masaa mawili.
Wachezaji wa timu ya Simba wakifanya  mazoezi maalum ya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, mechi uliyopewa jina la Nani matani Jembe.
KOCHA wa Simba, Patrick Phiri, amesema atakuwa na kikosi cha kwanza cha uhakika masaa mawili kabla ya kuanza kwa pambano la leo Jumamosi dhidi ya Yanga, lakini amethibitisha kuwa wachezaji wa kimataifa kutoka Uganda, Dan Sserunkuma na Emmanuel Okwi lazima waanze kwenye kikosi hicho.
Phiri aliongeza kuwa bado hatma ya kiungo, Jonas Mkude, kucheza kwenye mechi hiyo ya Nani Mtani Jembe ipo kwa daktari ambaye hadi jana Ijumaa alikuwa hajatoa uamuzi wa mwisho kama kiungo huyo acheze ama la.

Simba na Yanga zinakutana Uwanja wa Taifa katika mechi ya pili ya namna hiyo kuandaliwa na mdhamini wao, bia ya Kilimanjaro.
Katika mechi ya kwanza mwaka jana, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Phiri alikiri kuwa pambano hilo ni mtihani mkubwa wa mwisho kwake kutokana na mwenendo mbovu wa kikosi cha Simba msimu huu, lakini anaamini atashinda mchezo huo ili kurejesha imani yake Msimbazi.

“Unafahamu namna pambano la Simba na Yanga linavyokuwa, ni ngumu kusema nani atacheza na nani atakaa nje, uhakika utakuwapo masaa mawili kabla ya mchezo, mambo mengi yanaweza kutokea kati ya muda huu (jana Ijumaa) na kesho (leo Jumamosi),” alisema kocha huyo Mzambia.

“Kikubwa ni kwamba nilikuwa naangalia uwezekano wa kati ya Okwi na Sserunkuma mmoja acheze winga na mwingine straika namba mbili, wote ni lazima wacheze japo bado sijaamua yupi atacheza wapi.

“Uzuri mmoja ni kwamba wote wanaweza kucheza winga na pia straika wa kati, pia Okwi amepona maumivu ya enka yaliyomsumbua kwenye mechi za ligi, natarajia atacheza vizuri zaidi kwenye mchezo huu.

“Kuhusu Mkude bado hatujafahamu kama atakuwepo ama atakaa nje, nasubiri ripoti ya daktari lakini pia tayari nina mpango mbadala endapo atakosekana, itatulazimu kubadilisha mfumo ili kuendana na wachezaji nilio nao.”

Endapo Mkude atakosekana kwenye mchezo huo, Phiri atalazimika kubadili mfumo ili awapange viungo wakabaji wawili kuziba nafasi yake.

Kiraka Awadh Juma na kiungo Pierre Kwizera wataweza kuanzishwa kwa pamoja ili kusaidia safu hiyo ya kiungo, hivi ndivyo Mwanaspoti linavyofahamu.

Kama Simba itapotea mchezo huo hali inaweza kuwa mbaya kwa Phiri.
www.theheadliner24.blogspot.com

No comments

Powered by Blogger.