KASI YA DK JOHN MAGUFULI KUPAMBANA NA WATU WASIO WAJIBIKA YATIKISA KILA KONA YA NCHI, NI BAADA YA........

Kasi aliyoanza nayo Rais John Magufuli ya kupambana na watu wasiowajibika kwenye ofisi za umma, imeanza kutikisa sehemu nyingi baada ya taasisi tofauti kutoa maagizo ya kuongeza ufanisi, huku nyingine zikieleza ni kwa jinsi gani zimeitikia wito huo.

Wakati Wizara ya Afya na baadhi ya taasisi zake zikitoa maelezo ya kushughulikia vifaa vya tiba vilivyokuwa vibovu kwa muda mrefu, Wizara ya Madini imeeleza ni jinsi ilivyochukua hatua za kuongeza uwajibikaji, huku Wizara ya Habari ikihimiza utendaji na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni akifungua kituo cha kusikiliza kero za wananchi.

Rais Magufuli alikuwa akihimiza wakati wote wa kampeni yake kuwa wavivu na wazembe waanze kukusanya virago na baada ya kuapishwa, alitembelea Wizara ya Fedha, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kufanya kikao na makatibu wote wa wizara kutoa mwelekeo wa “Serikali ya Magufuli”, ikiwa ni pamoja na kusitisha safari za nje na kukusanya kodi bila ya upendeleo. Pia, aliiondoa Bodi ya Muhimbili pamoja na kaimu mkurugenzi na kuteua mpya, uamuzi ambao unaonekana kuzua taharuki kwenye taasisi za umma.

Jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Donan Mmbando aliwataka viongozi wote wa hospitali nchini kutoka maofisini na kusikiliza shida za wagonjwa na kuwaeleza huduma zinazotolewa kwenye vituo vyao vya afya na kwamba wazembe watachukuliwa hatua.

Dk Mmbando aliwaambia wanahabari jana baada ya kutembelea Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), kuwa mpango huo wa kutoa huduma bora wataufanya kwa kushirikiana na Tamisemi.

Katika kuanza kutekeleza mabadiliko hayo, Dk Mmbando aliagiza Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kutenga kiwango maalumu cha dawa kwa ajili ya kutibu wagonjwa wa saratani wa ORCI na kuhakikisha hospitali hiyo haikosi dawa.

“Ni mwisho kuanzia sasa kusikia mgonjwa wa saratani anasumbuliwa kwenda kununua nje wakati tunaweza kuweka utaratibu mzuri na dawa zikapatikana ndani ya hospitali,” alisema.

Alitoa agizo hilo baada ya kuelezwa na wagonjwa pamoja na menejimenti kuwa taasisi hiyo haina dawa na wagonjwa kununua kwenye maduka binafsi.

Mmoja ya wagonjwa waliolazwa ORCI, Felix Kessy alisema kwa sasa huduma zinaendelea vizuri hospitalini hapo, lakini ukosefu wa dawa unawalazimisha kwenda kununua mitaani ambako baadhi huuzwa kati ya Sh18,000 na Sh28,000.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk Diwani Msemo alisema ukosefu wa dawa ni changamoto kubwa kwa kuwa hospitali hiyo inatoa matibabu bure hivyo ni vigumu kukabiliana na uhaba huo.

Alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha wa jana 2014/15, Serikali ilipanga kuwapatia Sh6 bilioni kununua dawa, lakini wamepokea Sh2 bilioni tu.

Katika kukabiliana na tatizo la kifedha, Dk Mmbando aliagiza hospitali zote nchini kutumia sera ya ubia baina ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) katika kutekeleza miradi ambayo itasaidia kutatua matatizo.

“Kusiwe na sababu ya kumiliki kifaa tiba kama Serikali. Kuwe na makubiliano ya namna fulani ili mtengenezaji wa kifaa husika awe ndiyo mhudumiaji ila kitakuwa kikifanya kazi saa 24,” alisema.

Mwenendo wa CT-Scan ya Muhimbili

Kuhusu mashine ya kuchukua vipimo ya CT-Scan iliyoko Muhimbili, alisema tatizo hilo litatatuliwa na mafundi waliopo Uholanzi na kwamba ndani ya siku mbili itaanza kufanya kazi.

Ili kuzuia hali iliyojitokeza Muhimbili ya kuharibika vifaa, Dk Mmbando aliagiza hospitali zote ziwe na mpango kinga wa kutengeneza mitambo yao na zipange bajeti maalumu za matengenezo kwa kuwa wanakusanya mapato.

Alisema wameshailipa kampuni ya Philips Sh3 bilioni kati ya Sh7 bilioni wanazodaiwa kwa ajili ya matengenezo ya mashine hizo nchi nzima na kwamba wanaamini kwa sasa wataendelea kuhudumiwa bila kikwazo chochote.

Muhimbili yaingia hasara

Wakati hayo yakiendelea, Hospitali ya Muhimbili imeshindwa kukusanya zaidi ya Sh225 milioni katika muda wa siku 75 ambazo mashine za uchunguzi wa magonjwa za CT Scan na MRI zilikuwa mbovu kuanzia Agosti.

Ubovu wa mashine hizo umezuia huduma kwa zaidi ya wagonjwa 50 kwa siku ambao hufanyiwa uchunguzi hospitalini hapo na hivyo kufanya idadi ya wagonjwa waliokosa huduma hiyo kufikia 3,750.

Akizungumza na vyombo vya habari hospitalini hapo jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha alisema vipimo vya CT Scan vilikuwa vinatoa huduma kwa wagonjwa 40 hadi 60 kwa siku na hutakiwa kulipia Sh50,000.

Alisema MRI ilikuwa ikitoa huduma kwa wagonjwa 10 hadi 15 kwa siku kwa gharama ya Sh100,000 kila mmoja anayetumia kadi za bima za afya, wakati wanaolipia hutozwa Sh150,000.

Mashine hizo zilitakiwa kufanyiwa matengenezo na kampuni ya Philips lakini hayakufanyika kutokana na deni.

Wakati huohuo, mfanyabiashara wa Dar es Salaam, Mohamed Razak Dewji ametoa msaada wa vitanda 30 na magodoro 30 kwa hospitali hiyo ili kusaidia kupunguza adha ya wagonjwa kukosa vitanda.

Profesa Ole Gabriel na ‘Hapa Kazi Tu’

Kwingineko, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Profesa Elisante Ole Gabriel jana alitembelea mitambo ya kurushia matangazo ya Shirika la Utangazaji Tanzania(TBC) iliyoko Kisarawe mkoani Pwani kwa lengo la kufahamiana na wafanyakazi na akawahimiza kufanya kazi kwa bidii

Profesa Elisante alitembelea taasisi tatu zilizo chini ya wizara hiyo ambazo ni Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Shirika la Magazeti la Serikali (TSN) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ikiwa ni kutimiza kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu”.

Jana, Mwananchi ilishuhudia pilikapilika kwenye baadhi ya ofisi za umma, ikiwamo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Nishati na Madini.

Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud alisema watumishi wa wizara hiyo wapo tayari kufanyiwa ziara ya kushtukizwa kwa kuwa wanafanya kazi muda wote wa kazi.

“Hata Rais akija sasa hivi atakutana na ‘Hapa Kazi Tu’ wakati wa kazi. Kinachoendelea hapa wizarani ni uchapaji wa kazi. Kila mtu anatekeleza wajibu wake kwa vitendo,” alisema.

Katika kuonyesha hayo yanatendeka taasisi zilizo chini ya wizara hiyo zimeagizwa kutochelewa kushughulikia maombi ya wawekezaji wanapoonyesha dhamira ya kuwekeza nchini.

Agizo hilo amelitoa wakati wa kikao chake na watendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) pamoja na mwenyekiti wa bodi ya taasisi hiyo.

Makonda, Natty wakoleza moto

Kasi hiyo ya Dk Magufuli haijatikisa wafanyakazi pekee.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda na mkurugenzi wa manispaa hiyo, Mhandisi Mussa Natty jana walitoa maelekezo ya utendaji kazi na ufuatiliaji wa matatizo ya wananchi kwenye eneo lao.



Makonda, ambaye mara baada ya kuteuliwa alitenga muda kwa kusikiliza matatizo ya ardhi wilayani kwake kila Ijumaa, jana alizindua namba ya simu itakayotumika kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua.

Wakazi wa Kinondoni na wengine wanaotaka huduma wilayani humo, watatakiwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno kwenye namba hiyo na kueleza tatizo walilonalo na itapokewa na wafanyakazi maalumu watakaokuwa na kazi ya kuushughulikia.

“Tunatazamia kupunguza vitendo vya rushwa sambamba na kuongeza ufanisi kwa watumishi. Zamani kulikuwa na masanduku ya maoni, lakini hivi sasa hayapo tena. Kwa kutumia namba 15404 wananchi watawasilisha malalamiko yao sehemu salama,” alisema Makonda.

Alisema wapokeaji ujumbe huo watawasiliana na wakuu wa idara husika ili washughulikie kero hizo.

Wakati Makonda akizindua huduma hiyo, Natty, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kupokea msaada wa dawa za kipindupindu na vifaa tiba vilivyotolewa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), alitumia dakika zisizozidi sita kwenye shughuli hiyo akitaka watu kurejea kazini.

“Kila mtu anajua kuwa sasa tupo katika kipindi gani. Hapa ni kazi tu. Hatupaswi kupoteza muda katika vikao,” alisema. “Amri si ya kuzuia kusafiri nje pekee, bali kukaa mikutano isiyo na tija pia haitakiwi. Hivyo tunapaswa kulimaliza hili na kuendelea na shughuli zetu za utendaji wa kazi kama kawaida.”

Baada ya kusema hayo, Natty aliutaka ujumbe wa taasisi hiyo kumkabidhi msaada huo jambo lilofanywa kwa haraka na Mkurugenzi wa Fedha, Mipango na Uwekezaji, Deusdedit Rutaza aliyesema msaada huo wenye thamani ya Sh5 milioni unahusisha dawa za ugonjwa wa kipindupindu, glovu na dawa kuzuia mazalia ya wadudu katika mitaro ya maji machafu.

“Shughuli imeisha,” alisema. “Kila mfanyakazi arudi ofisini kwake mara moja. Nitakuja kukagua kama kila mtu anafanya majukumu yake. Muda wa kuzungukazunguka haupo tena.”

Wafanyakazi wazungumza

Dereva wa Wizara ya Nishati na Madini, Derick Samson alisema wafanyakazi wengi wanafika ofisini mapema kufanya shughuli zao, jambo ambalo ni tofauti na hali ilivyokuwa awali. Alisema wafanyakazi walikuwa wanafika ofisini muda wowote bila kuulizwa.

Mhudumu wa mapokezi wa Hazina, Beatrice Mvungi alisema wapo wanaolalamikia mabadiliko hayo.

No comments

Powered by Blogger.