NYIN GINE KUTOKA KWA DK. MAGUFULI, AAGIZA FEDHA ZILIZOANDALIWA KWAAJILI YA SHEREHE KUMPONGEZA ZIPELEKWE MUHIMBILI
Baada ya kulihutubia na kulizindua bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt JOHN POMBE MAGUFULI amehudhuria hafla fupi iliyoandaliwa kwa ajili ya wabunge katika viwanja vya Bunge Mjini Dodoma na kuagiza fedha zilizochangwa kwa ajili ya kugharamia hafla hiyo zipelekwe Katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kununulia vitanda vya wagonjwa.
Mheshimiwa Magufuli ametoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa kuwa wadau mbalimbali wamechanga kiasi cha shilingi milioni 225 kwa ajili ya kugharamia hafla ya wabunge katika siku ya uzinduzi wa Bunge.
Dkt Magufuli amesema alipata taarifa za kuwepo kwa michango hiyo ya fedha na kutoa maelekezo kuwa zitumike kwa kiasi kidogo kwa ajili ya hafla hiyo na sehemu kubwa zipelekwe katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili zikatumike kununulia vitanda na hivyo kupunguza tatizo la wagongwa wanaolala chini kutokana na uhaba wa vitanda unaikabili hospitali hiyo.
“Nilipoambiwa kwamba zimechangwa shilingi milioni 225 zimekusanywa kwa ajili ya sherehe, nikasema fedha hizo zipelekwe katika hospitali ya Taifa Muhimbili zikasaidie kununua vitanda” alisema Dkt Magufuli na kusisitiza kuwa “kwa kufanya hivyo tutakua tumejinyima sisi wenyewe lakini tutakua tumewanufaisha wenzetu ambao wanamatatizo makubwa yanayoweza kutatuliwa kwa fedha hizo”.
Awali akitoa taarifa ya michango hiyo Ofisa wa Spika wa Bunge Bwana SAID YAKUBU amesema jumla michango iliyopatikana na shilingi milioni 225 na kwamba fedha zilizotumika katika hafla hiyo ni shilingi milioni 24 tu baada ya kuzingatia maagiza ya Rais Magufuli.
Katika Hafla hiyo Rais Magufuli amekabidhi vyeti vya kutambua mchango wa wadau waliochangia fedha wakiwemo Benki za NMB, CRDB na Benki ya Afrika pamoja na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PSPF na PPF.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano IKULU
November 20, 2015
No comments