UMOJA WA MATAIFA WAANDIKA HISTORIA MPYA HUKU UJUMBE WA TANZANIA UKIONGOZWA NA RAIS DKT JAKAYA KIKWETE
VIONGOZI wakuu wa nchi na serikali zaidi ya 150 kutoka mataifa mbalimbali duniani (leo) Septemba 25,watapitisha ajenda na malengo mapya ya maendeleo endelevu (Ajenda 2030) kuchukua nafasi ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) yanayomaliza muda wake mwishoni mwa mwaka huu.
Katika mkutano huu wa kihistoria unaofanyika miaka kumi na tano tangu MDGs zilipopitishwa, utatanguliwa na hotuba ya Baba Mtakatifu Francis. Baada ya kupitisha ajenda 2030 na ambayo imejikita zaidi katika kuutokomeza umasikini na ulinzi wa mazingira pasipo kumwacha yeyote nyuma,viongozi hao kila mmoja wao atapata fursa ya kuelezea matarajio ya serikali yake katika utekelezaji wa ajenda hiyo yenye malengo 17.
Tayari viongozi hao wamekwisha wasili Jijini New York , yaliko Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa. Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
Siku moja kabla ya kupitishwa kwa ajenda 2030, baadhi ya viongozi ambao wameambatana na Rais Kikwete walishiriki katika mijadala mbalimbali ambayo maudhui yake yanashabihiana na ajenda nzima ya Maendeleo Endelevu.
Akiwakilisha ujumbe wa Tanzania katika mikutano hiyo ya pembezoni, Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula, alishiriki katika majadiliano kuhusu mabadiliko ya tabia nchi na uendelevu wa usalama wa chakula, lishe na afya.
Balozi Mulamula alikuwa kati ya wanajopo watano katika majadiliano hayo ambayo aliandaliwa na Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Ujerumani na Mashirika ya Kimataifa.
No comments