KUELEKEA UCHAGUZI MKUU KAULI ZA KULINDA TUNU YA AMANI ZIWE DIRA.
KAULI za Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Dk Mohamed Gharib Bilal pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein za kuwataka Watanzania kuendeleza amani, upendo na mshikamano, katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, Oktoba 25 mwaka huu, hazina budi kutekelezwa kwa vitendo.
Viongozi hawa wakuu wa kitaifa waliitoa kauli hizi wakati wa hotuba zao kwenye sherehe ya Sikukuu ya Idd el Haj jana. Dk Bilal alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo zilizofanyika kitaifa katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara, huku Dk Shein akiwa mgeni rasmi katika Ukumbi wa Chuo cha Amali Mkokotoni, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Dk Bilal alisema, Watanzania hawapaswi kuichezea amani iliyopo kwa namna yoyote ile, badala yake akawaomba kuilinda na kuiendeleza, huku akisisitiza kuwa, maendeleo ya nchi yoyote duniani yanategemea amani.
Aliongeza pia kwamba mshikamano na upendo sanjari na haki, ni msingi wa maendeleo na kuwaomba viongozi wa dini kuyapa vipaumbele katika misikiti na makanisa yote nchini. Dk Bilal pia akawakumbusha viongozi wa dini kuwa wana wajibu wa kuisaidia Serikali, iwapo watahubiri amani katika makanisa na misikiti kwani haitatumia gharama nyingi kujenga magereza, vituo vya polisi na badala yake itatumia gharama hizo kuzielekeza katika shughuli za maendeleo kwa wananchi wake.
Aidha aliwataka viongozi wa dini kuwahimiza waumini wa madhehebu yao, ifikapo Oktoba 25 mwaka huu wajitokeze kwa wingi kupiga kura kuwachagua viongozi waadilifu watakaoletea maendeleo wananchi na taifa kwa ujumla.
Aliongeza kuwa, kila Mtanzania ana wajibu wa kufuata sheria taratibu na kanuni za nchi hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu kwani matukio mengi ya umwagaji damu hutokea pindi kunapokosekana amani na haki, huku akiwaomba wanasiasa kufanya kampeni zao kwa mujibu wa sheria za nchi na Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) kwa Tanzania Bara na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Wakati Dk Bilal akisema hayo, Dk Shein alisisitiza kwamba Serikaili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kukabiliana na wale wote watakaofanya vitendo vitakavyoashiria kutaka kuvunja amani ya nchi wakati wote hasa katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Dk Shein aliwahakikishia wananchi kuwa hakuna atakayeonewa au kudhulumiwa kwa njia yoyote ile, lakini ni vizuri wajue kuwa Serikali ina wajibu wa kikatiba wa kuwalinda watu wote na mali zao.
Tunasema kauli hizo zichukuliwe kwa uzito mkubwa kwani amani tuliyonayo imewezekana kwa vile, viongozi wote waliotangulia na waliopo madarakani wameweka misingi iliyo bora na Watanzania wana wajibu wa kuilinda pia.
Tunaamini kwamba kila Mtanzania atatafakari kauli hizi kwa vitendo, kwani kama alivyosema Rais Shein, Serikali haijalala na haitalala, la msingi, ni kila mmoja kuzingatia sheria na kuachana na vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani ambapo yeyote anaweza kujikuta mikononi mwa dola badala ya kwenda kupiga kura kwa amani hapo Oktoba 25 ili kumchagua kiongozi amtakaye.
CREDITY: HABARI LEO
No comments