DUU!!!!! KUMBE... KOMBA NI MNYAMA MLEVI ANAEWAVUTIA WAGENI.

MUNGU ameumba ulimwengu na kujaza viumbe wenye tabia zinazotofautiana zikiwemo za kuvutia, kutisha na kushangaza kwa kuzingatia asili uhalisia wa viumbe wenyewe, na mazingira wanapoishi.
Binadamu ni miongoni mwa viumbe hao lakini anatofautiana na viumbe wengine kwa muonekano, tabia, makazi na mambo mengine mengi ingawa wengine wana tabia zinazofanana na mwanadamu. Baadhi ya tabia za wanyama zinazoweza kufananishwa na za binadamu ni zinazoingiliana kwenye vyakula. Inadaiwa kwamba, kwa mfano, binadamu akiwa porini akakosa chakula anashauriwa kumchunguza nyani ili kubaini anachokula myama huyo kwa sababu ndicho anachostahili kula hata yeye asidhurike.
Nyani na Sokwe ni miongoni mwa wanyama wenye tabia zinazofanana na tabia za binadamu, lakini komba anaonekana amepata umaarufu zaidi ya hao kutokana na tabia yake ya ulevi. Mhifadhi na mwongozaji wa wageni kwenye Hifadhi ya Wanyama Ifisi, Stanley Kiduko anasema, wageni wengi wanaotembelea hapo wanapendelea kutembezwa eneo la korongo ambako wanaishi wanyama wakubwa kama vile swala pala, swala grand, pofu, nyumbu na pundamilia.
Ingawa kuna wanyama hao, komba amekuwa kivutio kikubwa katika eneo hilo. Kiduko anasema wageni wengine hawapendi kwenda korongoni hivyo wanatumia darubini kuona wanyama hao na wengine ambao si rahisi kuwafikia karibu kwa sababu wana tabia ya kujitenga na uwoga. Anasema hifadhi hiyo ina korongo kubwa linalotokana na bonde la ufa.
Kiduko anasema, eneo hilo limehifadhi uoto wa asili, mabwawa ya maji na vichaka vyenye majani mabichi na kivuli kinachowavutia wanyama kupumzika wakati wa jua kali. Kiduko anasema, hifadhi hiyo imekuwa msaada kwa jamii ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, wanafunzi wa vyuo vya utalii katika ukanda huo wanaitumia kufanya mazoezi ya vitendo hivyo kuwapunguzia gharama za kuyafanya hayo nje ya eneo hilo.
Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo cha Loyal tawi la Mbeya, Verdiana Mathias anafanya mazoezi kwenye hifadhi hiyo na anamchambua kwa kifupi komba. Anasema, komba ni mnyama mwenye ukubwa kama paka, ana uzito wa gramu 150 hadi 1.5 Kg. Mwanafunzi huyo anasema, mnyama huyo akibeba mimba ana uwezo wa kuzaa mtoto mmoja au wawili baada ya siku 100 hadi 133.
Komba anapozaliwa macho yake yanaanza kuona kati ya siku sita mpaka nane, na kwamba, baada ya mwezi tangu kuzaliwa anaanza kufundishwa mazingira ya kujitegemea. Mathias anasema, komba anakula wadudu, wanyama wadogowadogo, matunda na maganda ya miti. Mnyama huyo anaishi kati ya miaka 12 hadi 16.5. Anamtaja Komba kuwa ni mnyama anayekaribiana na tabia za wanyama wenye tabia za binadamu.
Anasema, mnyama huyo anaipenda familia yake na kuilea kwa upendo. Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo, komba ni mlevi na anakunywa pombe za aina zote. Anasema mnyama huyo ni mchangamfu mara tu baada ya kunywa pombe lakini pia ana tabia ya kulia kama binadamu mtoto. Mathias anasema komba amekuwa akilia usiku na kwamba kilio hicho kinahusishwa na imani za uchuro kwa binadamu.
Kuna imani kwamba, komba akilia usiku kuna uwezekano siku inayofuata litokee jambo lisilo la kawaida kwa binadamu kikiwemo kifo. Imani hiyo pia inamhusu bundi. Mwanafunzi Eva Peter ambaye pia anasoma utalii kwenye Chuo cha Loyal tawi la Mbeya, anajifunza kwa vitendo kwenye hifadhi ya Ifisi. Peter anasema, mbuni ni ndege mwenye manjonjo na ni kivutio kikubwa kwa wageni wanaofika kwenye hifadhi hiyo kujionea maajabu ya wanyama na viumbe wengine.
Anasema, mbuni ana umbo kubwa, ana vidole viwili kwenye miguu yake yote miwili, ni ndege mwenye uwezo mkubwa wa kukimbia umbali wa kilomita 70 kwa dakika 30. Kwa mujibu wa Peter, mbuni jike ana uzito kati ya kilo 63 hadi 130 wakati dume uzito wake ni 156.8 Kg. Anasema, ndege huyo anaweza kuishi miaka 40 hadi 45. Dume ana shingo ya urefu wa mita 1.7 hadi mita 2 na jike urefu wa shingo yake ni mita 1.8 hadi 2.75.
Anasema, macho ya mbuni yana uwezo wa kuona umbali wa sentimita tano usawa wa kitu anachokitazama. Mwanafunzi huyo anasema, yai la mbuni ni sawa na mayai 25 ya kuku na kwamba, anaanza kutaga akifikisha umri wa miaka miwili hadi mitatu. Peter anasema, mbuni anataga mayai na kufukia kwenye udongo laini ili yasishambuliwe na viumbe wengine na nyakati hizo ndizo anazokuwa mkali kuliko kipindi kingine.
Anasema, mbuni anaishi katika mgawanyiko wa makundi kati ya 5 hadi 50, anakula pumba na wadudu wadogowadogo wakiwemo panzi. Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo, ndege huyo anapokutazama ana kwa ana anaitumia shingo yake kuonesha mbwembwe na manjonjo ya kunesanesa, hiyo ni sehemu ya maringo yake sawa na warembo wanavyoonesha miondoko yao jukwaani.
Anasema, mbuni jike ana manyoya yenye rangi ya kijivu ,wakati wa mchana yanafanana na vichaka hivyo kusababisha maadui wasimuone kwa urahisi anapolinda eneo alipotaga. Peter anasema, dume la mbuni linatumia rangi yake nyeusi usiku kuatamia mayai siku 21, na pia rangi hiyo ni kinga ili asionekane kirahisi. Mwanafunzi huyo pia anataja sifa za fisi wa nchi kavu wa madoa ‘kulukuta kulukuta’, kuwa ana miguu mifupi ya nyuma na kwamba anapatikana bara la Asia na Afrika.
Anasema, fisi dume ana uzito kati ya kilo 40.5 hadi kilo 55 wakati jike ana kilo 44.5 hadi 63.9. Peter anasema, mnyama huyo anabeba mimba kwa miezi 12 hadi 18, anazaa mtoto mmoja au wawili kwa wakati mmoja na anaishi miaka 20 hadi 25. Anasema, chakula kikubwa cha fisi ni nyama ambayo sehemu kubwa ni mifupa na ndiyo maana wakati wote kinyesi chake kama chokaa. Kwa mujibu wa Peter, fisi hawapendi nyama laini wala vyakula vingine.
Kwenye hifadhi hiyo fisi wanalishwa vichwa vya ng’ombe, mbuzi na miguu. “Kwa kawaida fisi ni mlafi, hawa watatu tulionao hapa tumewazoeza kuwapa kichwa kimoja, wana uwezo wa kula zaidi ya hapo kwa siku, ukiwaendekeza ni gharama sana. Wana uwezo wa kula hata ugali lakini si asili yao wakati mwingine kama ni ugali wanaweza kunusa na kuacha,” anasema Peter.
Anasema, mnyama huyo ana uwezo wa kunusa umbali wa zaidi ya kilomita moja, na anapenda kucheka, ni mwoga ila si mnyama rafiki wa wanyama wapole. Peter anasema, fisi jike anaanza kupandwa akiwa na umri kati ya siku 90 hadi 110. Mwanafunzi mwingine wa chuo hicho anayefanya mazoezi kwa vitendo katika hifadhi hiyo, Betty Chaula yeye anamzungumzia pofu.
Anasema, mnyama huyo ni mpole, anavutia, ni mnyama rafiki wa wanyama wapole na anapenda kuishi kwenye vichaka vifupi na sehemu za mabwawa. Mwanafunzi huyo wa mwaka wa kwanza anasema, mnyama huyo ana kimo cha sentimita 200 mpaka 2800. Chaula anasema, pofu jike ana uzito kati ya kilo 300 hadi 600 wakati dume ana uzito wa kilo 450 mpaka 1,000.
Anasema, mnyama huyo ana uwezo wa kuishi kati ya miaka 15 na 20 na anapatikana nchi za Angola, Ethiopia, Namibia na Tanzania. Chaula anasema, pofu anakula majani na anapenda sehemu za wazi zenye vichaka vifupi. Anasema, mnyama huyo anaanza kupandwa akiwa na miaka kati ya minne hadi mitano, anabeba mimba na kuzaa baada ya miezi minane. Chaula pia anataja sifa za pundamilia.
Anasema, mnyama huyo anayepatikana Tanzania, kaskazini ya Kenya, eneo la milima la Ethiopia, na kusini magharibi ya Afrika mwenye mvuto kumtazama ana uzito wa kilo 350 na anakula majani. Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo, pundamilia anaishi kwenye vichaka vifupi, anabeba mimba kwa miezi 13, na anapandwa akiwa amefikisha umri wa miaka mitatu.
Anasema, mnyama huyo anaishi kati ya miaka 20 hadi 25, ni mpole anapenda kujichanganya kwenye makundi ya wanyama wapole lakini ni mnyama anayejitenga wakati wa kulea. Mwandishi wa makala haya ni msomaji wa HabariLeo.

No comments

Powered by Blogger.