SIKU MBILI KABLA YA UCHAGUZI VIPEPERUSHI VYA KUTISHIA USALAMA VYA SAMBAA.
Siku 2 kabla ya siku ya uchaguzi mkuu
kufanyika, watu wasiojulikana wamesambaza vipeperushi kwenye mitaa ya
manispaaya Mtwara Mikindani, vikitishia asipochaguliwa mgombea ubunge wa
chama cha wananchi– CUF toka umoja wa katiba ya wananchi– UKAWA kwa
jimbo la Mtwara mjini, nyumba zao zitachomwa moto.
Wakitoa taarifa juu ya vipeperushi hivyo kwenye kikao kati ya jeshi
la polisi, viongozi wa vyama vya siasa na waandishi wa habari, baadhi
ya washiriki wa kikao hicho wamesema, walianza kuviaona vipeperushi
hivyo mitaani kuanzia majira ya alfajiri, vikiwa na maneno hayo ya
kutishia usalama, wakati taifa likielekea kufanya ucahguzi mkuu, na
hivyo kuliomba jeshi la polisi kufuatilia vipeperushi hivyo, kwani
havina nia njema kwa wananchi wa mkoa huo.
Alipoulizwa juu ya madai hayo, mgombea ubunge wa chama cha
wananchi–CUF kwa kivuli cha umoja wa katiba ya wananch – UKAWA jimbo la
Mtwara mjini Maftaha Nachuma ambae ametajwa kwenye vipeperushi hivyo,
amekanusha kushiriki kuvifahamu, akidai kitendo hicho kimefanywa na
wapinzani wake, kwa lengo la kumchafua yeye, chama chake na umoja wa
katiba ya wananchi - UKAWA.
Kwa upande wake, kamanda wa polisi mkoani Mtwara kamishna msaidizi
wa polisi Henry Mwaibambe amesema, polisi inayo taarifa juu ya
vipeperushi hivyo, ambapo amedai, vingine vimekutwa vimetupwa kwenye
eneo la makazi ya jeshi hilo, na hivyo polisi imeanza uchunguzi juu ya
wahusika wa tukio hilo, huku akiwataka wananchi wa mkoa huo kutokuwa na
hofu, kwani polisi ipo makini kudhibiti hali ya amani mkoani humo.
Credity: ITV
No comments