BOSSOU ATAKA AAMINIWE JANGWANI
BAADA ya kuanza kuzoea mikikimikiki ya Ligi Kuu nchini, beki wa kimataifa wa Togo anayeichezea Yanga, Vincent Bossou, amemtaka kocha wake Hans van der Pluijm, kumwamini na kumpa nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza.
Bossou ni mmoja wa wachezaji ghali kwenye kikosi cha Yanga msimu huu, lakini muda mwingi amekuwa akikalia benchi huku Pluijm, akiendelea kuwatumia wazawa Kelvin Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Akizungumza na gazeti hili, Bossou, alisema shauku yake kubwa ni kuona kocha anampanga kwa sababu anajiamini ana uwezo wa kumudu ushindani uliopo kwenye ligi na uthibitisho ni katika mechi mbili alizoichezea timu hiyo na kuonesha kiwango cha juu.
“Kocha amenisifia katika mechi mbili nilizocheza nadhani kwa sasa anapaswa kuniamini na kunipanga kikosi cha kwanza kwa sababu naamini nina uwezo wa kuhimili ushindani uliopo na kuisaidia timu yangu kupata mafanikio,” alisema Bossou.
Beki huyo alisema kwa muda mrefu aliokuwa benchi amejifunza mambo mengi kuhusu soka la Tanzania na hakuna kitakachomsumbua pindi atakapoaminiwa na kuonesha uwezo wake.
Alisema anajua Yanga ni timu kubwa na muda wote mashabiki wake wanahitaji ushindi na ubingwa na yeye analifurahia hilo na yupo tayari kushirikiana na wenzake kwa ajili ya kuipa mafanikio timu hiyo.
Bossou ametua Yanga akitokea timu ya An Giang ya Vietnam na beki huyo anaichezea timu yake ya taifa ya Togo inayofundishwa na kocha wa zamani wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet.
No comments