KERR KUTAKIWA NA WATOTO WA JANGWANI

KOCHA wa timu ya soka ya Simba, Dylan Kerr ameutaka uongozi wa timu hiyo kuhakikisha unamwongezea mkataba beki wake wa kulia Hassan Kessy kutokana na mchango mkubwa aliokuwa nao.
Kessy ataruhusiwa kufanya mazungumzo na timu nyingine ifikapo Desemba mwaka huu wakati ambapo atakuwa amebakiza miezi sita ya kuitumikia Simba kwenye mkataba wake wa sasa, huku Yanga ya Dar es Salaam ikitajwa kumwania kwa udi na uvumba.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kerr alisema Kessy ni mchezaji mwenye kipaji cha juu na bado angependa kuendelea kufanya naye kazi kutokana na mchango wake Simba.
“Mchango wake mkubwa tumefunga mabao mengi kutokana na krosi zake hicho ni kielelezo tosha kwamba huyu ni mchezaji anayestahili kuendelea kubaki na sisi,” alisema Kerr.
Hata hivyo, alisema bado hajapata nafasi ya kuzungumza na mchezaji huyo, lakini ameutaka uongozi wa Simba kuhakikisha unapambana kumbakisha.
Alisema anataka kuendelea na Kessy kutokana na uzoefu aliokuwa nao kwenye Ligi ya Tanzania Bara, tofauti na Mrundi Emery Nimubona, ambaye pamoja na uwezo aliokuwa nao ameshindwa kuonesha ushindani kwa mzawa huyo.
Beki huyo ameripotiwa katika siku za karibuni kwamba yupo mbioni kuachana na Simba, huku timu za Yanga na Azam zikitajwa kumwania.

No comments

Powered by Blogger.