MIKOA MINNE KUFAIDIKA NA MRADI WA KUSAMBAZIWA GESI MAJUMBANI KAMA UMEME JE, NI MKOA WAKO.... BASI SOMA HAPA UJUE
WANANCHI 37,900 wanatarajia kuanza kunufaika na matumizi ya gesi majumbani pamoja na magari 9,400 kwa kuunganishwa na matumizi ya gesi kwenye mikoa minne inayopita bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka jijini Dar es Salaam.
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pia limesema gesi itaanza kuzalisha umeme wa megawati zaidi ya 40 mkoani Pwani pamoja na kutumika katika viwanda mbalimbali.
Akizungumzia usambazaji wa gesi katika mikoa minne ya Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Salaam,bMkurugenzi wa Usafirishaji, Usafishaji na Usambazaji wa gesi katika Mkondo wa chini, Dk Wellington Hudson alisema pia watasambaza gesi katika kiwanda cha saruji mkoani Mtwara.
Alisema katika mkoa wa Pwani eneo la Mkuranga kuna ujenzi wa viwanda mbalimbali, kikiwemo cha uzalishaji umeme katika eneo la Bagamoyo na wako katika mazungumzo na kampuni ya Kamar kujenga bomba la gesi kufika Bagamoyo.
Hudson alisema katika eneo la Mzinga wanategemea kuzalisha umeme wa megawati zaidi ya 40 kwa ajili ya matumizi ya viwandani kulingana na mahitaji ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) utakaogharimu Dola za Marekani milioni 20.
Akizungumzia mkoa wa Mtwara, alisema usambazaji utakuwa wa mtandao wa kilometa 100 ambapo wananchi 900 wa matumizi ya gesi majumbani watanufaika huku magari 400 yatatumia gesi na tayari upembuzi yakinifu umekamilika.
Kwa upande wa mkoa wa Lindi, alisema mtandao wake ni kilometa 17 ambapo wateja 7,000 wa matumizi majumbani watanufaika na watumiaji 1,000 wa magari tayari upembuzi yakinifu na michoro tayari kwa ujenzi imekamilika.
Alisisitiza kuwa katika mkoa wa Dar es Salaam mtandao utakuwa wa kilometa 65 ambapo wateja wa kutumia gesi majumbani watakuwa 30,000 huku magari 8,000 yakitumia gesi na sasa fedha zinatafutwa kujenga miundombinu tayari upembuzi na michoro imekamilika.
No comments