RAIS WA NIGERIA DARASA KWA MAGUFULI

HATIMAYE, Jumapili iliyopita, Watanzania walipiga kura kumchagua Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge na madiwani. Bila kujali walioshindwa au kushindwa, mchakato mzima wa uchaguzi huo kufanyika kwa amani tangu mwanzo hadi mwisho ni ushindi mkubwa kwa nchi yetu. Hatuhitaji kuangalia mbali kutambua hatari zinazoandamana na chaguzi hususan barani Afrika, ambao, kwa mfano, wenzetu wa Burundi hadi leo bado wanapitia kipindi kigumu baada ya mchakato kama huo tulioumudu. 





Ni vigumu kufanya Uchaguzi Mkuu usio na kasoro za hapa na pale. Hiyo si kwa huko nyumbani tu bali hata huku kwa wenzetu ambao kwa kiasi kikubwa ni wazoefu wa demokrasia. Uchaguzi Mkuu uliofanyika hapa Uingereza, Mei mwaka huu, pia ulitawaliwa na kasoro za hapa na pale, licha ya matumizi ya hali ya juu ya teknolojia ya kisasa. Kwa hiyo, tunastahili kujipongeza kwa hatua tuliyofikia. Hata hivyo, wakati taarifa mbalimbali za wasimamizi wa uchaguzi huo, wa ndani na wa nje, zikibainisha kuwa ulikuwa wa huru na haki, kinachoendelea huko Zanzibar ni cha kusikitisha. Katika huu mji ninaoishi wa Glasgow hapa Uskochi, kuna idadi kubwa ya Watanzania kutoka Zanzibar, na moja ya mambo yaliyonifadhaisha ni kuona sie Wabara tuna furaha ya kumalizika kwa uchaguzi kwa amani lakini wenzetu hao wa Visiwani wakiwa na hofu ya hatma ya uchaguzi huo, kwa upande wa Zanzibar. 




Kuna maswali kadhaa kuhusu kilichojiri huko Zanzibar lakini kwa vile jitihada za kutatua utata huo zinaendelea basi sina mengi ya kujadili kwa sasa isipokuwa kutoa rai kwamba tatizo hilo linapaswa kutazamwa kama la kitaifa na si kiitikadi, kuliangalia kama tatizo la upande mmoja wa Muungano wetu na sio upinzani kati ya CCM na CUF. Kwa upande mwingine, matokeo ya uchaguzi huo mkuu, ambao mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli alimbwaga mpinzani wake mkuu, mgombea wa Ukawa, Edward Lowassa, yamethibitisha kile kilichousiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, kuwa ili mabadiliko ya kweli yapatikane, na ili upinzani ufanikiwe kuing’oa CCM madarakani, kunahitajika mikakati makini itakayohusisha watu makini.
Baadhi yetu hatukueleweka tulipomtabiria Magufuli ushindi mapema huku wafuasi wa Lowassa wakitutuhumu kuwa tumenunuliwa na CCM. Ukweli mchungu ulikuwa mwepesi; uchaguzi wa mwaka huu ulifanyika katika mazingira yale yale ambayo wapinzani walishindwa huko nyuma kuishinda CCM. Ukiachia vyama vinne kushirikiana na kusimamisha mgombea mmoja wa urais, na tukiweka kando ujio wa Lowassa huko upinzani, sambamba na Waziri Mkuu mwenzake wa zamani, Frederick Sumaye, kimsingi fursa ya vyama vya upinzani kuishinda CCM ilikuwa finyu. Kinachosikitisha sasa ni kuona baadhi ya Watanzania wenzetu hawataki kukubaliana na ukweli kuwa Lowassa kashindwa, na Magufuli sio tu ameshatangazwa kuwa Rais wa Tano wa Tanzania bali pia ataapishwa rasmi. Kuna hadaa zinaendelea, hususan huko katika mitandao ya kijamii kuhusu ‘rufani ya Ukawa.’ 
Japo wana-Ukawa wana haki ya kulalamikia kasoro walizoziona katika uchaguzi huo, lakini ni vema kutambua kuwa Katiba yetu ipo wazi: hakuna mamlaka inayoweza kumvua Magufuli urais. Wafuasi wa Lowassa na Ukawa wana uchaguzi mmoja tu, kukubali kuwa wameshindwa, kwamba kuwa na matarajio makubwa pasipo mikakati thabiti ya kugeuza matarajio hayo kuwa uhalisia ni kujiandalia maumivu tu mbele ya safari, na pia kuna maisha baada ya uchaguzi. Ni vema wajitathmini na kujiandaa kwa chaguzi zijazo za mbele. Kwa upande wa ushindi wa Magufuli, licha ya kumpongeza kwa ushindi wake, ningependa kumkumbusha ahadi yake aliyoirudia mara kadhaa; “Sitowangusha.” Nina imani, yeye binafsi na chama chake kimepata fundisho kubwa kutokana na uchaguzi huu, na ni matarajio ya wengi kuwa Rais Magufuli atafanya kila awezalo kurekebisha matatizo mbalimbali yanayokikabili chama chake na taifa letu kwa ujumla. Hotuba aliyotoa baada ya kukabidhiwa cheti cha kushinda nafasi ya urais imeleta matumaini kwa wengi. Katika hotuba hiyo, Rais- mteule Magufuli alieleza bayana kukerwa kwake na usaliti uliokigubika chama chake wakati wa kampeni za uchaguzi huo, na alikwenda mbali zaidi na kumkosoa Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, kwa kutochukua hatua dhidi ya wasaliti waliomzunguka. Baadhi yetu tumetafsiri kauli hiyo ya Magufuli kuwa ni dalili ya kutowaonea aibu watendaji wanaoboronga mambo. Kama kuna kipaumbele kikubwa kabisa kwa urais wa Magufuli ni mapambano dhidi ya ufisadi ambao almanusura uigharimu CCM. Laiti Ukawa wasingejiloga na kumteua Lowassa, mwanasiasa waliyemtuhumu kwa muda mrefu kuhusu ufisadi, kuwa mgombea wao, na wangesimamia ajenda yao ya kupinga ufisadi, basi huenda muda huu tungekuwa tunaongea lugha nyingine. Ujio wa Lowassa huko Ukawa ulipelekea wanasiasa mahiri katika mapambano dhidi ya ufisadi kusinyaa na kukwepa kuzungumzia suala hilo linalogusa hisia za Watanzania wengi. Mtihani wa kwanza kwa Magufuli ni uteuzi wa baraza lake la mawaziri. Lakini mtihani huo unaweza kuwa mwepesi iwapo ataamua kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya chama pekee. Inatarajiwa atakaowateua kuwa mawaziri wake wawe wachapakazi kama yeye na sio tu kutokana na nafasi zao katika chama chake. Kadhalika, asikubali kuburuzwa kwani pindi mambo yakienda mrama, wa kulaumiwa atakuwa yeye na sio waliomburuza. Jingine ni haja ya baraza la mawaziri dogo lililojaa wachapakazi. Ukubwa wa baraza la mawaziri sio tu ni mzigo wa walipakodi bali hutoa fursa kwa watendaji wazembe kujificha kwenye migongo ya wenzao. Kwa bahati nzuri, Magufuli anaingia madarakani akiwa na bahati ya uwepo wa sehemu ya kujifunza. Na sehemu hiyo si nyingine bali ni kinachojiri nchini Nigeria baada ya Rais Muhammad Buhari kuingia madarakani. Wengi walidhani jenerali huyo mstaafu angeendeleza ‘business as usual’ lakini kuna dalili nzuri kuwa amepania kwa dhati kupambana na tatizo la rushwa sambamba na kusimamia uwajibikaji kwa viongozi wa serikali. Ilimchukua Buhari muda mrefu kidogo kabla hajakamilisha safu ya kabineti yake kwa sababu alipania kuwa na kundi la watendaji watakaomwezesha kuitumikia nchi hiyo kwa ufanisi. Kwa hiyo, si lazima Magufuli atangaze kabineti yake mapema iwapo atahitaji muda zaidi wa kujenga kikosi imara cha wachapakazi. Nimalizie makala hii kwa kukumbusha tena umuhimu wa kutafuta suluhu ya mgogoro wa kisiasa unaoendelea huko Zanzibar. Hatuwezi kuwa na furaha kamili ya kumaliza uchaguzi upande mmoja wa Muungano ilhali upande wa pili wanaishi kwa hofu na kutojua hatma yao. La muhimu kabisa ni kuweka kando itikadi za kisiasa katika utatuzi wa mgogoro huo, na badala yake kutanguliza maslahi ya taifa letu. Mwisho nimpe hongera nyingi kwa Dk. Magufuli kwa ushindi wake ambao unathibitisha imani ya Wtanzania kwake. Kama alivyowaahidi kuwa hutowaangusha, ninamsihi atafsiri ahadi hiyo kwa vitendo. Mungu ibariki Zanzibar, Mungu ibariki Tanzania - See more at: http://www.raiamwema.co.tz/rais-wa-nigeria-darasa-kwa-magufuli# SOURCE RAIA MWEMA

No comments

Powered by Blogger.