JE, HISTORIA YA MAPINDUZI NA UMWAGAJI DAMU KUJIRUDIA?

KUFUTWA kwa matokeo ya Uchaguzi Zanzibar na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo (ZEC) hapo Oktoba 28 mwaka huu, kwa madai ya kuwa na kasoro nyingi ni mzengwe unaofanya historia ya machafuko yaliyosababisha Mapinduzi ya umwagaji damu ya Januari 12, 1964 kujirudia.
Akitangaza kufuta uchaguzi huo, Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, alitaja sababu tisa, zikiwamo wajumbe wa tume kutofahamiana; wajumbe kuvua mashati na kupigana kwenye chumba cha kutangazia matokeo; kura zilizopigwa kuzidi kwa baadhi ya majimbo ya uchaguzi hasa Pemba; mmoja wa wagombea wa urais kujitangazia ushindi kabla ya matokeo na sababu zingine.
Hatua hiyo haikushitua umma wa Kitanzania tu, bali jumuiya ya kimataifa pia, wakiwamo waangalizi wa kimataifa, waliokiita kitendo hicho kuwa “cha kusikitisha kwa uchaguzi [kama] huo uliofanyika vizuri na kwa amani”.
Marekani kwa upande wake, kupitia ubalozi wake jijini Dar es Salaam, ililaani kitendo hichoikisema, “hatua ya ZEC inakwenda kinyume kabisa na tathmini ya waangalizi wa uchaguzi kutoka ubalozi wake, Jumuiya ya Ulaya (EU), Jumuiya ya Madola na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kuwa uchaguzi huo ulikuwa wa haki”.
Mtafaruku uliozushwa na ZEC si wa kwanza kwa siasa za Zanzibar, bali ni mwendelezo wa mitafaruku kama hiyo, kuanzia enzi za harakati za kudai uhuru mwaka 1957 hadi Mapinduzi (1964) na miaka ya karibuni kufikia kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) mwaka 2010.
Mwaka 1958, wakati uhasama kati ya vyama vya ukombozi visiwani – Afro-Shirazi Party (ASP) na Zanzibar Nationalist Party (ZNP) ulipofikia kilele na kutishia umoja na hivyo kuathiri harakati za ukombozi, Rais wa kwanza wa Ghana, hayati Dk. Kwame Nkrumah, aliwaita na kuwakalisha chini mjini Accra, viongozi wa vyama hivyo, Abeid Amani Karume (ASP) na Ali Muhsin (ZNP) na kufikia mwafaka wa kwanza wa kudumisha umoja, uliojulikana kama “The Accra Accord”, lakini mwafaka huu ulivunjika baada ya mwaka mmoja tu wakati harakati zikiendelea na uhasama kurejea kama mwanzo.
Chaguzi zote zilizofanyika kati ya mwaka 1959 na 1963 zilitawaliwa na mizengwe dhidi ya ASP, na kwa ZNP kulelewa na kukingiwa mbawa na Serikali ya Sultani chini ya udhamini wa Wakoloni wa Kiingereza walioitawala Zanzibar tangu mwaka 1890.
Baadhi ya njama zilizofanywa na serikali dhidi ya ASP ni pamoja na wafuasi wa chama hicho kutishwa na kukamatwa ovyo ili kutia hofu miongoni mwao; kuongezwa kwa majimbo ya uchaguzi kwenye maeneo yenye wafuasi wengi wa ZNP ili kuongeza viti vya ushindi; wizi wa kura na mara nyinginekufutwa kwa matokeo pale ASP ilipoonekana kupata ushindi mkubwa.
Lengo la yote haya lilikuwa ni kukihakikishia ushindi Chama cha ZNP (na baadaye Muungano wa ZNP na Zanzibar and Pemba Peoples’ Party – ZPPP) kilichodai uhuru kwa madhumuni ya nchi kubakia chini ya himaya ya Sultani kama zilivyo Canada, Australia na nchi zingine, ambazo licha ya kuwa nchi huru, lakini zinabakia kuwa chini ya Himaya ya Malkia wa Uingereza Kikatiba.
Kwa chaguzi zote kuelekea uhuru, mara nyingi ASP kilishinda kwa wingi wa kura lakini kilihujumiwa. Vivyo hivyo, katika uchaguzi wa mwisho uliofanyika Julai 1963, ASP kilishinda kwa wingi wa kura zilizopigwa lakini kikashindwa kwa viti vya Bunge kwa kupata viti 11, na Muungano wa ZNP/ZPPP (Ukawa) ukapata viti 13 na kukabidhiwa serikali, Desemba 10, 1963, chini ya Waziri Mkuu Mohamed Shamte wa ZPPP kutoka Pemba.
Serikali ya Shamte, iliyoonekana kutowakilisha wala kukidhi matakwa halisi ya Wazanzibari, ilidumu kwa mwezi mmoja tu hadi Januari 12, 1964, pale ilipopinduliwa na wanaharakati wa ASP na wenzao wa Chama cha Umma Party (UP) cha Abdulrahman Babu.
Kufuatia Mapinduzi hayo, Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, alitangaza kwamba kusingekuwa na uchaguzi Zanzibar kwa miaka 50 mfululizo hadi 2014 kwa madai kwamba dhana ya uchaguzi ni jambo la kikoloni. Pia, iliazimiwa kwa Hati ya siri [na ambayo inaelekea inaendelea kusumbua siasa za Zanzibar] kwamba, chini ya utawala wa ASP, wote waliokuwa wafuasi wa ZNP na ZPPP na ndugu zao hadi vizazi, na hasa wenyejiwa Visiwa vya Pemba [alikotoka Shamte na Othman Sharrif], wasipewekamwe nafasi za uongozi katika Serikali ya Mapinduzi na [baadaye baada ya Muungsano, 1964] katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kama njia ya kuwakomoa kwa siasa zao za upinzani dhidi ya ASP.
Ubaguzi huu umeitesa jamii ya Kizanzibari kwa nusu karne sasa. Kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa lengo la kutuliza uhasama huo kumesaidia kwa kiasi fulani kuleta amani na utulivu Zanzibar.
Hata hivyo, hali na historia ya uhasama wa kisiasa Visiwani vinaonekana kujirudia kwa misingi na kwa mbinu zile zile za miaka ya 1960 kufuatia kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992 nchini na hivyo kufumua upya vidonda/majeraha ya kale.
Katika chaguzi kuu zoteza mwaka 1995, 2000na2005, na hata huu wa 2015, Chama cha Wananchi (CUF) ambacho ni Chama Kikuu cha Upinzani Visiwani, kimedai kila mara kupokonywa ushindi kwa hila na CCM mithili ya ASP kilivyopokonywa ushindi kila mara na ZNP/ZPPP miaka ya 1950 – 1960.
Matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 30, 2000, kama yalivyokuwa matokeo ya Januari 1961, yalifuatiwa na vurugu na machafuko ya kisiasa ambapo watu 30 waliuawa na vyombo vya dola; wakati mwaka 1961 watu 69 waliuawa na zaidi ya 100 kujeruhiwa; bila kuhesabu walioikimbia Zanzibar.
Hali kama hii ndiyo iliyoshinikiza kuundwa kwa tume ya pamoja ya Rais, mwaka 2001 ili kupendekeza mwafaka wa Kitaifa, kama ilivyokuwa mwaka 1958 kwa kutiwa sahihi Mwafaka wa Accra – “Accra Accord”.
Juhudi hizi za kutafuta mwafaka kwa njia ya SUK, zilifanyika katikati ya kauli tete za wapinga Umoja wa Kitaifa, kama aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CCM (taifa) Ramadhan Mapuri, ambaye aliwahi kutamka hadharani kwa kusema, “Uhuru wa Zanzibar ulipatikana kwa mapanga, hivyo hauwezi kukabidhiwa kwa yeyote yule kwa njia ya sanduku la kura”; akimaanisha kwamba, hata kama Chama chochote cha upinzani kitashinda, CCM Zanzibar haiko tayari kuyatambua matokeo, wala kukabidhi Serikali kwa mshindi asiyetokana na zao la ASP, kwa sasa CCM Zanzibar.
Mapuri hakuwa peke yake kwa hilo, kwani hata Rais wa Awamu ya sita ya Serikali ya Zanzibar, Amani Abeid Karume, aliwahi kutoa tamko kama hilo aliposhinda uchaguzi 2005, kwamba, “CCM Zanzibar haina historia, wala Zanzibar haiwezi kuwa na utamaduni wa kuunda Serikali ya Mseto na Chama chochote”; na kuongeza kwamba, “kama lolote lisilotarajiwa (kushindwa uchaguzi?) litatokea, tuko tayari kutumia silaha za Mapinduzi ya 1964 kwani CCM Zanzibar inazo funguo za silaha hizo”.
Ni kutokana na shinikizo la Jumuiya ya Kimataifa, pamoja na Serikali ya Muungano chini ya Rais Jakaya Kikwete kwa kuitaka Zanzibar iachane na siasa za uhasama kwa maridhiano kwa njia ya SUK, mwaka 2008, Rais Karume alikiambia kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM iliyoketi Butiama kwa kiburi akisema: “Vikao vya CCM havina mamlaka ya kuwaamulia Wazanzibari jinsi ya kutawala nchi yao”; lakini katika hali ya kuonekana kulainika alisema, “…hata kama Wazanzibari wataamua, Serikali ya Mseto haiwezi kuja kabla ya 2010.
Hata hivyo, kufikiwa kwa Mwafaka mpya kwa njia ya SUK mwaka 2010 halikuwa jambo rahisi wala la hiari. Baraza la Wawakilishi lililokutana Machi 2010, lilipitisha Azimio lililoweka msingi wa SUK na upatikanaji wake kwa njia ya kura ya maoni na kura hiyo ilipigwa Julai 31, 2010 ambapo asilimia 71.7 ya Wazanzibari wenye haki ya kupiga kura walishiriki.
Matokeo yalikuwa kwamba, asilimia 64.4 ya kura zilikubali kuundwa kwa SUKkuashiria kwamba Wazanzibari walikuwa wamechoshwa na ubaguzi na uhasama wa kijinga wa enzi za kale.
Oktoba 31, 2010, uchaguzi wa Rais ulifanyika katika hali ya amani na utulivu kuliko chaguzi zote katika historia ya Zanzibar. Uchaguzi huo ndio uliozaa Serikali ya Mseto ambapo mshindi, Dk. Ali Mohamed Shein, aliyepata kura nyingi zaidi aliteuliwa kuwa Rais, na aliyefuata kwa vyama vya upinzani, Maalim Seif sharrif Hamad wa CUF, aliteuliwa Makamu wa kwanza wa Rais.
Februari 28, 2011, Serikali ya Marekani, kupitia Balozi wake nchini, Alfonso Reinhardt, iliipongeza Kamati ya Maridhiano iliyofanikisha kufikiwa kwa mwafaka huo, chini ya Mwenyekiti wake na aliyekuwa kada mkongwe wa CCM, Mzee Hassan Nassoro Moyo, kwa kuitunuku tuzo ya “Martin Luther King Drum Major”.
Akipokea tuzo hiyo kwa niaba ya tume, Mwenyekiti wa CCM wa Baraza la Mapinduzi, Ali Mzee Ali, alielezea sababu za uamuzi wa Wazanzibari wa kukubali kuunda SUK, akisema; “Uongozi wa viongozi wote wa Zanzibar kutoka CCM na CUF, waliweza kusoma alama za nyakati ndani ya wakati kuepuka Mapinduzi kama yale yanayotokea Afrika Kaskazini ….Zanzibar tayari ni taasisi na mfano wa demokrasia wa kuigwa na nchi zingine”.
Kumbe, hofu ya machafuko na pengine Mapinduzi ya umwagaji damu ndiyo iliyosababisha kuundwa kwa SUK; bila hivyo hali ya kisiasa Zanzibar ingeendelea kubakia ile ile ya ubaguzi na uhasama wa kihistoria.



Kwa Zanzibar, kusimikwa kwa mifumo ya kisiasa kwa njia ya shinikizo si kitu kigeni. Mwaka 1964, kufuatia Mapinduzi ya Kikomunisti ya Januari 12, mwaka huo, nchi za Magharibi, zikiongozwa na Marekani na Uingereza ziliingiwa hofu ya Ukomunisti kuikumba Afrika kupitia Zanzibar katika kipindi hicho cha vita baridi duniani.
Juhudi za awali za nchi hizo zilikuwa ni kuhakikisha kuundwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki (EAF) ili Zanzibar iweze kumezwa ndani ya Shirikisho pana isifurukute. Kazi ya kuratibu Shirikisho hilo alipewa Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere.
Na pale juhudi za kuunda EAF ziliposhindwa, nchi hizo za Magharibi, kwa pamoja ziliandaa mkakati wa kuivamia Zanzibar kijeshi, chini ya mpango ulioitwa “Zanzibar Action Plan” (ZAP) na amri ya kufanya hivyo ilikuwa mbioni kutolewa.
Ni Mwalimu Nyerere aliyeokoa siku, pale alipoziomba nchi hizo kusitisha ZAPili madhumuni na kusudio la EAFiliyokusudiwa kuhusu Zanzibar, lifanywe na kutekelezwa na Tanganyika ili Visiwa hivyo viweze kumezwa ndani ya tumbo pana la Tanganyika (ili Ukomunisti udhibitiwe) kwa njia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Hofu ya Mwalimu ilikuwa ni kuona vita kati ya Mataifa makubwa ya Magharibi [nchi za Kibepari] na ya Mashariki (Ukomunisti – Urusi na China) vikipiganwa mlangoni mwa Tanganyika. Ni Marekani na Uingereza zilizosimamia na kuratibu mchakato mzima wa Muungano, na wakati mwingine kwa njia ya vitisho, hadi “Tan-Zan-ia” ikapatikana.
Na hivi karibuni, ni Marekani iliyotoa ushawishi na msukumo kufikiwa kwa SUK mwaka 2010 ili kujihakikishia hali ya utulivu na amani kwa uwekezaji wake Visiwani na Tanzania kwa ujumla, hasa katika sekta ya mafuta na gesi. Angalia jinsi kampuni ya mafuta na gesi yalivyokuwa yakipigana vikumbo kwa utafiti Zanzibar na Pwani yote ya Tanzania: Shell, BP, Antrim, Amoco, Texaco na Ophir. Mengine ni British Gas, Tullow, Artumas, Maurel & Prom, Statoil na mengine mengi.
Ili kuweza kuwekeza kwa tija, kulitakiwa hali ya amani na utulivu Visiwani badala ya kuendelezwa kwa ugomvi wa kijadi kati ya CCM Zanzibar na CUF Zanzibar. Na hiyo ndiyo moja ya madhumuni ya kuundwa kwa SUK.
Sasa, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imetupilia mbali uchaguzi ambao tayari matokeo yake yalionesha Mgombea wa CUF, ameshinda kiti cha urais. Jumuiya ya Kimataifa nayo imethibitisha kwamba uchaguzi huo ulikuwa ni wa haki na kwamba sababu za kufutwa kwake hazina mashiko. Marekani kwa upande wake, imekwishatoa msimamo wake. Je, italifumbia macho jambo hili na kuhatarisha vitega uchumi vya kampuni zake?
Hofu ya ZEC iliyopelekea kufuta uchaguzi ni ipi? Je, dhana ya SUK ina maana gani kwa Zanzibar kama uchungu ni kwa mwanadamu pekee (CCM) na mkuki ni kwa nguruwe pekee?
Mawili haya yana majibu katika tamko chafu la Mapuri kwamba, “Uhuru wa Zanzibar hauwezi kukabidhiwa kwa yeyote kwa njia ya sanduku la kura”.
ZEC inatakaje ili haki kwa wote ipatikane? Na huu uhafidhina na uhasama wa kale wenye kuchafua amani na hivyo kukaribisha nguvu ya mataifa makubwa mlangoni kwetu mithili ya enzi za vita baridi unatoka wapi zama hizi za mahusiano ya kimataifa, haki za binadamu na utawala bora? Tutafakari. - See more at: http://www.raiamwema.co.tz/historia-ya-mapinduzi-ya-umwagaji-damu-kujirudia#sthash.SOURCE RAIA MWEMA

No comments

Powered by Blogger.