HABARI ZA MITANDAONI ZICHUJWE KABLA YA KUSAMBAZWA....

WAKATI Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli ikiendelea kuchapa kazi kwa kasi, lipo jambo linalotia doa juhudi hizo za serikali, nalo ni kukithiri kwa uzushi, unaotia doa dhamira hiyo ya serikali ya kubadili mifumo katika utendaji serikalini.
Katika kile kinachoonesha kuwa pengine ni kutokana na kufurahia kupita kiasi kwa kazi nzuri inayofanywa sasa na Serikali, hasa Rais, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue na hata Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, watumiaji wa mitandao wameanza kupenyeza taarifa za uzushi au za kweli, lakini zikiwa zimetiwa chumvi kupitiliza na hivyo kuharibu mboga.
Watumiaji wasio waaminifu wa mitandao, wameanza kuwatisha watendaji wa taasisi mbalimbali za umma na zisizo za umma, kwa kuandika na kutawanya mambo yasiyo na ushahidi juu ya taasisi hizo, hatua ambayo si nzuri sana kwani inatia doa na kupunguza imani kwa wananchi kuziamini taasisi na watendaji wa taasisi hizo.
Wakati huu ambapo Rais, Katibu Mkuu Kiongozi na Waziri Mkuu, wamekutana na watendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wizara ya Fedha, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na kuibua kashfa mbalimbali, ikiwemo upotevu wa mabilioni ya fedha za umma na uzembe, habari nyingi katika mitandao ya jamii, zimetawaliwa zaidi na utiaji chumvi wa matukio hayo.
Kwa mfano wapo watumiaji wa mitandao ya jamii, ambao bila ya kuwa na ushahidi wowote, wamekuwa wakiwashambulia watendaji wa taasisi za umma, ambazo bado Rais hajazitembelea kwa kuorodhesha madhambi mbalimbali, wakidai kuwa yamefanywa na watendaji hao, jambo ambalo si sahihi, kwani linapunguza kiwango cha imani waliyonayo wananchi kwa taasisi hizo na watendaji wake.
Kama hiyo haitoshi, wazushaji wa taarifa hizo za kimtandao, pia wamekuwa wakiwashambulia wafanyabiashara mbalimbali kwa kuwazushia tuhuma mbalimbali, lakini bila kutoa ushahidi, kinyume na matakwa ya sheria ya Makosa ya Mitandao, jambo ambalo si sahihi kwa vile linatia hofu na kurudisha nyuma nia njema ya serikali ya kuvutia uwekezaji.











Katika kile ambacho hakiwezi kuachwa kikaendelea kuvumiliwa, baadhi ya watumiaji wa mitandao hiyo ya kijamii, wamekuwa wakichukua hata nyaraka za Ikulu, kama taarifa kwa vyombo vya habari na kuzifanyia masahihisho ili kuweka taarifa za uongo ndani yake kwa lengo la kunogesha zaidi taarifa halisi, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa Taifa.
Pamoja na kufanya vitendo hivyo ambavyo vinazuiliwa na Sheria ya Makosa ya Mitandao, watumiaji hao wamekuwa wakizitawanya taarifa hizo katika mitandao hiyo kama facebook, twitter, whatsapp, u-tube, jamii forum na mingineyo, hatua ambayo inawafanya watu wengi zaidi wa ndani na nje ya nchi, kuchangia masuala ambayo hayana ushahidi.
Katika tukio la bahati mbaya sana, Watanzania pamoja na kujua kuwa wanafanya makosa, wamekuwa wakizisambaza taarifa hizo bila kuzichuja ili kujua ukweli na uhalali wake, hatua inayopanua zaidi wigo wa watu wanaoingia kwenye makosa, endapo mamlaka husika zitaanza kuchukua hatua stahiki na kwa uzito wake.
Naandika Wazo hili kama sehemu ya utoaji wa elimu kwa umma, kwa kuwaomba Watanzania kuacha tabia hiyo ya kueneza uzushi na badala yake wafanye hivyo kwa mambo yenye mantiki na ambayo hayawezi kurudisha nyuma kasi na jitihada za Rais, Katibu Mkuu Kiongozi na Waziri Mkuu katika kukabiliana na vitendo vya hujuma dhidi ya serikali.
Ni kweli mitandao ya jamiii, imekuwa tegemeo kubwa katika upashanaji wa habari kwa haraka na kasi ulimwenguni kote, lakini ni vyema watumiaji wakaitumia kusambaza taarifa zilizo sahihi na zilizothibitishwa na mamlaka halali ili kuondoa uwezekano wa kujenga taifa lenye hofu, hatua inayoweza kufifisha vita dhidi ya maovu ndani ya taifa letu.
Ni wakati muafaka sasa kwa Watanzania, kuanza kuchuja taarifa ili kupata usahihi wake kabla ya kuzisambaza ili kuondoa shaka za wananchi, ambao kadri siku zinavyozidi kwenda mbele wanazidi kupunguza imani kwa taarifa za mtandaoni kutokana na kushamiri kwa taarifa za uongo, au zilizotiwa chumvi kupita ukweli halisi.

No comments

Powered by Blogger.